Mbinu bora za kufundishia,
ni miongozo mbalimbali atumiayo mwalimu wakati wa kufundisha somo aliloliandaa
kwa wanafunzi wake. Walimu wanapaswa kuamua kwa kuchagua kwa makini njia na
mbinu bora za kufundishia ili wanafunzi wake waweze kujifunza kwa ufanisi. Ziko
njia nyingi za kutengeneza mazingira ya mtoto aweze kujifunza na pia ziko mbinu
nyingi za kufundishia. Pamoja na wingi huo tunaweza kuzigawa katika makundi
makuu mawili kadri ya jinsi zinavyowashirikisha watoto katika tendo la
kujifunza, ambazo tunaweza kuziita shirikishi
na zisizo shirikishi.
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu shirikishi na zisizo shirikishi za kufundishia pamoja na
faida na hasara zake:-
Njia ya majadiliano,
njia hii imekuwa ikitumika katika ufundishaji kwa muda mrefu. Katika
kujadiliana mwanafunzi mmoja mmoja hupata nafasi ya mawazo aliyonayo kuhusu
suala linalojadiliwa na yeye pia huweza kupata mawazo yaw engine. Katika
majadiliano mwanafunzi hupata ujuzi mpya nje na ule aliokuwa nao kabla
hajashiriki katika majadiliano.
Mambo ya kuzingatia.
· Kazi iwe na changamoto ya kutosha
kuhitaji majadiliano ili wahusika wafikie uamuzi wa pamoja.
· Kazi ilenge wahusika kutoa mawazo na
hatimae kupata ujuzi mpya kutokana na majadiliano.
· Yawepo malengo yanayoeleweka vizuri na yanayotekelezeka. Ni muhimu malengo
haya yawekwe wazi kwa wahusika.
Faida za mbinu.
Ø Kukuza mahusiano ya wahusika.
Ø Kuwafanya wahusika wafurahie na kulipenda somo.
Ø Kukuza stadi za ubunifu na mawasiliano.
Ø Kujenga uwezo wa wahusika wa kuamini na kuvumiliana.
Ø Huleta ujuzi na uongozi.
Ø Kila mmoja huweza kutoa mchango wake na mawazo yake kwani watu ni wachache katika
kundi.
Ø Husaidia kujenga kumbukumbu kwa wanafunzi.
Hasara za mbinu hii.
Ø Kama hakuna usimamizi na utaratibu mzuri njia hii inaweza isiwe tofauti na mhadhara
kwani mtu mmoja tu au kiongozi anaweza kutawala uwanja wa mazungumzo.
Ø Kama kiongozi si imara, kundi linaweza kushindwa kujadili mada waliopewa na hivyo
kujadili nje ya mada.
Ø Hujenga uhasama kati ya kundi na kundi, wanafunzi na wanafunzi.
Njia ya mhadhara,
hii ni njia ya kufundishia kitu kwa kutumia hotuba ndefu. Lengo la kutumia njia
hii ni kuwazoeza wanafunzi kuwa wasikivu na kuzingatia mambo muhimu na yenye
msingi tu kati ya maelezo mengi yanayotolewa na mhadhiri.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
· Njia hii itumike kwa wanafunzi
waliopevuka kimawazo.
· Njia hii itumike katika kuanzisha mada
mpya ikiwa tu itaonekana haipo njia nyingine ya kufundishia mada hiyo.
Faida za mbinu hii.
Ø Huwezesha kufundisha mambo mengi kwa wakati mmoja.
Ø Humjengea mwanafunzi tabia ya kuchambua taarifa na kuzingatia mambo muhimu tu.
Ø Inapima usikivu wa mwanafunzi kuhusu mada inayofundishwa.
Hasara za mbinu hii
Ø Haiwashirikishi sana wanafunzi katika tendo la kujifunza.
Ø Huwachosha wanafunzi kwa sababu watoto hawawezi kuwa wasikivu kwa muda mrefu.
Ø Wanafunzi huchoka kusikia sauti ya mtu mmoja tu muda wote.
Ø Ni mtu mmoja tu anayetoa mawazo yake na wengine yaani wanafunzi hupokea tu, hivyo
hujenga utegemezi kwa wanafunzi.
Kazi mradi,
wanafunzi na walimu wengi wameelekea kuamini kuwa mbinu ya kazi mradi ni ya
utendaji wa mda mrefu. Kwa wengi kazi mradi inatumika tu kwa kuwatathimini
wanafunzi kwa muda huo mrefu. Kwa mtazamo wa sasa kazi mradi yaweza kufanyika
hata kwa kipindi kimoja tu cha darasani. Katika utendaji wanafunzi huunda maana
zao binafsi kutokana na jinsi nadharia husika zinavyojitokeza katika maisha
halisi ya kila siku.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
· Mwalimu lazima abainishe kuwa anatumia
njia hii katika hatua gani ya mada husika na kuna umuhimu gani wa kutumia njia
hii na isiwe nyingine.
· Wanafunzi wapewe fursa ya kuchagua mambo
ya kufanya katika kazi mradi wakishirikiana na mwalimu.
· Wanafunzi wanatakiwa wajue nini cha
kufanya na utendaji wao unatakiwa uwe wa kiwango gani na kwa muda gani.
· Mwalimu wasaidie wanafunzi katika
kuunganisha taarifa na kuzijazia maana.
Faida za mbinu hii.
Ø Kukuza stadi mbalimbali za kufikiri.
Ø Kujenga tabia ya kuhusisha mambo wanayojifunza na maisha yao ya kila siku.
Ø Kujiamini na kupenda kujifunza kwa kujitegemea.
Hasara ya mbinu hii.
Ø Ni vigumu kuchagua mada ifaayo kufundisha kwa njia hii.
Ø Kama haikuandaliwa vizuri maarifa au ujenzi wa maana uliokusudiwa hushindwa
kuwafikia walengwa.
Njia ya ziara, hii ni safari inayopangwa kwa madhumuni fulani. Hii ni dhiara ya kielimu ambayo
hufanywa kwa njia ya kutembelea na kuona mahali ua vitu halisi kwa njia ya
kujifunza. Katika mazingira ya kishule waalimu hufanya ziara na wanafunzi wao
kutembelea sehemu mbalimbali zenye mambo yanayohusiana na mada wanazofundisha
shuleni. Wanafunzi wanaweza kutembelea sehemu kama vyanzo vya mito, madimbwi,
viwanda, benki, posta na mbuga za wanyama.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
· Mwalimu afanye uchunguzi wa kina kuhusu
sehemu ya kufanyia ziara kuona kama ina jambo linalokusudiwa kufundishwa.
· Yawekwe malengo ya ziara hiyo wazi kwa
kila mmoja.
· Kuamua iwapo watafanya kazi kwa vikundi
au mmoja mmoja na mwalimu agawe majukumu kwa kila mmoja au kila kundi.
· Mwongozo au maswali ya kusaidia kupata taarifa
zinazotakiwa zitolewe mapema kwa wanafunzi ili uwasaidie wakati wa ziara.
· Vifaa na jinsi ya kukusanya taarifa
wakati wa ziara. Vifaa kama daftari, kamera na vinasa sauti vinaweza
kutayarishwa.
Faida za mbinu hii.
Ø Humpa mwanafunzi nafasi ya kuwa katika mazingira halisi wakati wa kujifunza.
Ø Hufanya dhana dhahania kueleweka kwa kina zaidi.
Ø Huongeza motisha na kumuwezesha mwanafunzi kupenda kujifunza zaidi.
Ø Huondoa utata unaoweza kuwepo kutokana na mawazo ya awali ya wanafunzi na kuwafanya
wajenge dhana kamilifu zaidi.
Ø Hushirikisha wanafunzi wote.
Ø Wanafunzi hutegemea katika kupata taarifa inayotakiwa badala ya kumtegemea mwalimu.
Hasara ya mbinu hii.
Ø Gharama huwa kubwa – usafiri.
Ø Matayarisho huchukua muda mrefu.
Ø Usimamizi huwa mgumu hasa kama darasa lina wanafunzi wengi na mahali pa ziara ni mbali.
Ø Sio rahisi kuendesha somo kwa kipindi kimoja tu.
Onyesho mbinu, ni uwasilishaji unaofanywa wa matendo kuhusu jambo au dhana fulani. Onesho mbinu
huambatana na maelezo ya ana kwa ana, Matumizi ya zana na maswali na majibu
ambayo huwezesha wanafunzi kujifunza stadi mpya.
Mambo ya kuzingatia katika mbinu hii.
· Andaa dhana mahususi za somo au mada.
· Andaa vifaa vyote vinavyotakiwa katika
onyesho.
· Fanya zoezi la onyesho lako kabla ili
kuona kuwa onyesho lako linafanikiwa.
· Waeleze hatua zitakazo fuata katika
onyesho.
· Washirikishe wanafunzi wako kila mara na
kila hatua inayofanywa.
· Toa nafasi kwa wanafunzi kufanya onesho
wenyewe.
· Toa muhtasari wa maelezo kuhusu dhana
uliojifunza mala baada ya onesho.
Faida za mbinu hii.
Ø Kujifunza kwa kuona kuna mahamasisho makubwa katika kujifunza.
Ø Kujenga ari ya kujifunza.
Ø Wanafunzi hujifunza kwa kutenda chini ya kiongozi au mtaalamu.
Ø Njia hii huwezesha kufanya masahihisho ya moja kwa moja katika kujifunza.
Hasara za mbinu hii.
Ø Maandalizi makini hutakiwa na muda mwingi wa vitendo hutakiwa.
Ø Hairuhusu idadi kubwa ya wanafunzi.
Ø Maandalizi
mabaya yanaweza kupotosha maana ya onesho.
Kwa kuhitimisha, inaweza kusemwa kuwa mbinu au njia za kufundishia na kujifunzia ni
ujanja anoubuni mwalimu kila awapo darasani, kwa lengo la kurahisisha
uelewekaji wa somo husika katika tendo la ufundishaji na ujifunzaji. Hivyo basi
kila suala au jambo analolifanya mwalimu wakati wa somo darasani huweza kusemwa
kuwa ni mbinu au njia ya kufundishia na kujifunzia.
MAREJELEO
Ø Mgombele J.Mwiga (2003). Mbinu za kufundishia na kujifunza: mwandiga bookshop.
Ø Jiandae.wordpress.com/zana za kufundishia.
Ø Paulmeela.wordpress.com/mbinu za kufundishia Kiswahili.
0 $type={blogger}:
Post a Comment