SOMO LA 1: KUPITIA YA KITABU CHA DANIELI:
A; D A N I E L I:
Lengo la 1; - Eleza Historia fupi ya Danieli.
Danieli – jina lake lina maana “Mungu ndiye Hakimu wangu”. Alikuwa mmojawapo wa mateka waliochukuliwa na mfalme Nebukadneza katika mwaka 605 KK. Kutoka Yerusalemu na kupelekwa Babeli. Aliishi kipindi chote cha utumwa cha miaka 70 huku akiwa nabii na mwandishi wa Kitabu cha Danieli. Tunamfahamu Danieli jinsi alivyokuwa mcha Mungu, tukisoma Eze.14:14-20. Inavyoonekana alitokea na ukoo wa daraja la juu huko Yerusalemu. Danieli hakuwahi kuoa, inawezekana alifanywa towashi kwa sababu alifanya Kazi katika Kasri la mfalme.
B. KITABU CHA DANIELI:
Lengo la 2 : Taja tarehe na makusudi ya kuandikwa kitabu hiki.
Kitabu hiki kiliandikwa kati ya mwaka 536 – 530 KK. Kikiwa na makusudi mawili.
1. Kuwatia moyo mabaki huko Babeli kuwa utumwa ulikuwa sio mwisho wa taifa lao.
2. Kuwaonyesha watu wa Mungu kuwa Mungu ndiye mtawala wa mataifa yote.
-Yesu amekithibitisha kitabu kuwa kiliandikwa na Danieli.
Lengo la 3: Eleza mgawanyo wa Kitabu hiki:
Kitabu hiki kimegawanyika katika sehemu kuu tatu:
1. Historia fupi ya Danieli toka Yerusalemu hadi Babeli –(Dan. 1:1-21)
2. Ujumbe wa Danieli kuhusu utawala wa Mungu juu ya mataifa yote (2:1)
3. Maono ya Danieli (8:1 - 12:13)
Sura ya kwanza iliandikwa kwa lugha ya Kiebrania wakati sura zingine zimeandikwa kwa lugha ya Kiaramu.
Lengo la 4: Eleza mambo maalum ya kipekee yaliyomo katika Kitabu cha Danieli
Kitabu cha Danieli kina mambo ya kipekee nane. Nayo ni:-
- Kitabu kifupi kuliko vitabu vya Manabii wote ambacho watu wanasoma na kujifunza mno.
- Unabii wa Danieli umenukuliwa sana katika A/Jipya.
- Ni kitabu cha Apokilasi cha A/Kale kinachoelezea mambo ya siku za mwisho.
- Ni kitabu pekee kinachoelezea ujio wa kwanza wa Masihi katika Dan. 9:24-27
- Kinaelezea zaidi maisha ya Mwandishi, Tabia, Hekima na Maombi yake.
- Kina maombezi ambayo ni mfano wa maombezi ya kuwasamehe watu wa taifa lake kwa kumkumbusha Mungu ahadi zake.
- Habari za Danieli na rafiki zake zinapendwa mno.
- Maandishi yaluiyoandikwa na kutangaza yamekuwa methali inayotumiwa sana leo.
Lengo la 5: elezea Dola na mji wa Babeli na makusudi ya huduma ya Danieli.
Mji wa Babeli ulijengwa Kusini kando ya mto Efrata. Hali ya hewa na maumbile ya asili yalifanya mji wa Babeli uwe na watu wengi. Mfalme Nebopolasa alikuwa ndiye mwanzilishi wa Dola ya Babeli na kukuzwa sana na mtoto wake aitwaye Nebukadneza.
Dola ya Babeli ilipokuwa na nguvu ikaiangusha Ashuru na kuteka Palestina na Misri. Kutokana na 2Nyak. 36:15-17, Yuda ilichukuliwa uhamishoni kwa sababu waliacha sheria ya Bwana. Mungu akawahukumu watu wake kwa kuwaweka katika utumwa mikononi mwa Wakaladayo. Danieli aliinuliwa kuwa Nabii ili awatie moyo mabaki waliokata tamaa kuwa Mungu ndiye anamiliki na kuiongoza historia.
MASWALI:
- Kitabu cha Danieli kiliandikwa mwaka gani?
- Makusudi ya kuandikwa kwa kitabu hiki ni:
(a) _____________________________________
(b) _____________________________________
- Kitabu hiki kimegawanywa katika sehemu ngapi?. Zitaje.
- Taja mambo manne ambayo ni ya kipekee katika Kitabu hiki.
- Dola ya Babeli ilikua zaidi katika kipindi cha mfalme _______________
SOMO LA 2: UCHAMBUZI WA KITABU CHA DANIELI.
PAMBANO LA KWANZA MAPAMBANO DHIDI YA MASWALA YA IMANI (11-21)
Lengo la 1: Eleza pambano la kwanza la Imani la Danieli na rafiki zake.
Je, walishindanaje?, nini matokeo ya kushinda kwao?
Baada ya Danieli kufika Babeli, mfalme Nebukadneza aliamua Danieli na wenzake wapate elimu ya Ukaldayo kuhusiana na lugha na mila za Babeli. Hii itawafanya watumike vizuri. Ili kutimiza kusudi hili, mfalme Nebukadneza alifanya mambo yafuatayo:-
Kwanza: Aliwapa uraia wa Babeli kwa kubadili majina yao kama ifuatavyo:
Kiebrania:
- Danieli (Mungu ni Hakimu wangu – Belteshazzar (Mwana wa Bel)
- Hanania (Mungu ni mwenye Neema) –Shadrack (Uvuvio wa Rachi)
- Mishaeli (Nani kama Mungu) – Meshaki (nani kama Shaki)
- Azaria (Mungu anasaidia) – Abdinego (mtumishi wa Nebo)
Pili: Aliamua kuwapa vyakula ambavyo vilitolewa kwa miungu, ili wawe na afya nzuri. Katika hili, Danieli na wenzake waliamua kutojitia unajisi kwa kula vyakula vilivyotolewa kwa miungu. Wakaomba wale mboga na maji kwa muda wa siku kumi. Mungu akawajalia wakaonekana wana afya nzuri zaidi kuliko wenzao. Kwa ajili ya kumcha Mungu, Mungu aliwapa hekima na ufahamu katika masomo yao.
Je, tunajifunza nini kutokana na tabia, mwenendo, na Imani ya Danieli?
Msingi wa jaribu lao la kwanza ilikuwa ni kuwafanya hao Vijana waikane imani yao na kuishi kama Wababeli. Hawa vijana hawakukubali. Mara nyingi Jumuiya tunazoishi zinataka tufanane nazo bali kama watu wa Mungu tuishi kati yao tukiwa tunamcha Bwana.
PAMBANO LA PILI: UCHAWI DHIDI YA HEKIMA YA MBINGUNI (Dan. 2:1-49)
Lengo la 2: Tambua vitu vilivyokuwemo katika sanamu aliyoiona mfalme Nebukadneza.
Mungu alimwonyesha mfalme Nebukadneza ndoto iliyohusiana na falme mbalimbali zenye nguvu. Hizi falme zingehusika sana kwa Taifa la Israeli.
1. Kichwa cha Dhahabu – Dola ya Babeli (mamlaka) – Dan. 2:37
2. Kifua na mikono ya fedha – Dola ya Uajemi na Umedi (Serikali ya Seri) – Dan. 2:39.
3. Tumbo na viungo vya shaba – Dola ya Uyunani (utamaduni ) – 2:39
4. Miguu ya chuma – Dola ya Rumi – 2:39
5. Nyayo zilizo nusu chuma na nusu udongo – Jumuiya ya Mataifa 10 chini ya mpinga Kristo – 2:40
6. Jiwe lisilochongwa na mwanadamu – Ufalme wa miaka elfu wa Yesu Kristo – 2:42.
Lengo la 3: Eleza umuhimu wa ndoto ya Nebukadneza na Nyakati za Mataifa.
Sanamu hii inaelezea mambo yatakayotokea katika historia. Kipindi hicho ni kuanzia mfalme Nebukadneza hadi kurudi mara ya pili kwa Yesu Kristo. Nyakati za mataifa ni wakati nchi ya Israeli itakapokaliwa na mataifa mengine.
Pili, Ndoto hii ni muhimu kwani lilikuwa shindano kati ya uchawi dhidi ya Hekima ya Mungu. Mfalme Nebukadneza alitaka kukumbushwa ndoto aliyoota kwanza halafu aambiwe tafsiri. Wachawi walipoitwa walishindwa kuielezea na kuhukumiwa kifo. Katika mistari ya 17-28 tunaona hali nzuri ya Kiroho ya Danieli na rafiki zake.
- Walimwomba Mungu ili afunue ndoto hii (17,18)
- Walimshukuru Mungu baada ya kupata jibu (19-23)
- Walimpa utukufu Mungu katika yote (27,28)
Matokeo yake:-
(a) Mfalme Nebukadneza alitambua uwezo wa Mungu wa Danieli
(b) Danieli alipewa zawadi kubwa nyingi.
(c) Akapandishwa cheo cha Uliwali
(d) Rafiki zake nao wakaongezewa cheo.
Je, Tunajifunza nini katika pambano hili?
PAMBANO LA TATU: KUABUDU SANAMU DHIDI YA KUMWABUDU MUNGU
(Dan. 3:1)
Lengo la 4: Eleza matokeo ya ushindi wa vijana watatu wa Kiyahudi:
Mfalme Nebukadneza badala ya kunyenyekea na kumwabudu Mungu aliyemwonyesha ndoto hii, anaamua kutengeneza sanamu. Anaamuru watu wote waisujudie. Watu wote wanasujudu isipokuwa Shadrack, Meshaki na Abednego. Matokeo yanakuwa hivi.
- 8-12 – Viongozi wenzao wanawashtaki
- 13-15 – Mfalme Nebukadneza anawapa nafasi ya kutekeleza agizo ili kuepuka hukumu.
- 16-23 – Hukumu inatekelezwa kwa kutupwa kwenye tanuru la moto.
- 24-27 – Bwana anajifunua na kuwaokoa watu wake.
Matokeo ya ushindi huu unaleta mema:
(a) Mfalme Nebukadneza anamtambua Mungu kuwa ndiye amewaokoa.
(b) Watu wanaamriwa kutomnenea lisilopasa Mungu wa Shadraka, Meshaki na Abednego.
(c) Vijana hao watatu wakabandikwa vyeo.
Je, tunajifunza nini katika vita hivi?
Kuwa tayari kufa kwa ajili ya Yesu Kristo kuliko kumwasi Mungu kwa kuogopa mateso. Mungu mwenyewe ana uwezo wa kutuokoa katika mateso hayo.
PAMBANO LA NNE: KIBURI CHA MFALME DHIDI YA UTAWALA WA MUNGU.(Dan. 4:1-37)
Lengo la 5: Je, tunapata kweli gani katika Dan. 4?
Katika sura hii mfalme Nebukadneza anaeleza ushuhuda wake.
4:18 – Anaelezea ndoto yake ya mti uliokua sana na baadaye kukatwa.
19-27 - Danieli anaeleza tafsiri ya ndoto kuwa mfalme Nebukadneza kuondolewa ufalme na kula majani kama mnyama wa porini kwa miaka saba.
28-36 - Mfalme anaelezea kutimia kwa ndoto aliyoota
37 - Mfalme anamtambua Mungu.
Ukweli tunaopata hapa ni kuwa Mungu anahusika katika kung’oa na kuweka
Wafalme na viongozi mbalimbali. Je, tunapata fundisho gani?
(a) Kabla Mungu hajaleta hukumu humpa maonyo ili ajirekebishe
(b) Mungu hapendi mtu aliye na kiburi, hivyo humshusha.
PAMBANO LA TANO: KUFURU YA MWANADAMU DHIDI YA UTAWALA WA MUNGU (Dan. 5:1-31)
Lengo la 6: Eleza dhambi ya Belshazzar.
Karamu hii ilifanyika mwaka 539 KK, wakati wa mfalme Belshazzar.
Alitawala Babeli wakati baba yake Naboduis alikuwa anaongoza vita sehemu nyingine. Wakati huu mji ulikuwa umezingirwa na majeshi ya Wamedi na Waajemi. Matukio wakati wa karamu:
- Karamu yaandaliwa na watu wasifu miungu yao – 5:1,2
- Akiwa amelewa aagiza vyombo vya hekalu la Yerusalemu viletwe na kutumiwa –(Mst. 2-4)
- Kitanga chaandika maneno na wenye hekima kujaribu kusoma (Mst.5-8)
- Danieli aletwa kusoma na kutafsiri maandishi (Mst. 9-31)
Maandiko: MENE, MENE TEKELI , NA PERESI
MENE – Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha.
TEKELI – Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka.
PERESI – Ufalme wako umegawanyika nao wamepewa Waamedi na Waajemi.
Dhambi ya Belshazzar ilikuwa ni kufanya dhambi kwa makusudi kutumia vyombo vitakatifu vya hekalu la Yerusalemu. Alikuwa amesikia na kumfahamu Mungu huyo.
Je, tunajifunza nini? Tusifanye dhambi kusudi kwani tutakuwa tunamkufuru Roho Mtakatifu.
PAMBANO LA SITA: WIVU DHIDI YA BARAKA ZA MUNGU JUU YA MTU WAKE.(Dan. 6:1-28)
Lengo la 7: Eleza jinsi Mungu anavyowatetea watu wake.
Danieli anapewa uongozi tena katika ufalme wa Dario huko Babeli. Huyu Dario siyo yule mfalme mkuu anayetajwa katika Agano la Kale, huyu inawezekana alikuwa kiongozi aliyewekwa na mfalme Koreshi kusimamia utawala. Wawili waliomo katika Baraza la uongozi wanamwonea wivu Danieli kutokana na utendaji mzuri wa kazi. Matukio yanakuwa ifuatavyo:
- Wanamshawishi mfalme kuandaa sheria ya kutokuomba kwa Mungu ila kwa mfalme kwa siku 30. (4-9)
- Daniel aendelea kuomba na akamatwa na kutupwa katika tundu la simba(10-17)
- Mungu amwokoa Danieli na maadui kuadhibiwa (18-24)
Matoke ya ushindi wa Danieli mfalme Dario anawataka watu kumheshimu Mungu wa Danieli. Pia Danieli akaendelea kufanikiwa.
Je, tunajifunza nini katika sehemu hii?
Mtu anapomtegemea Mungu, Mungu humfanikisha na kukutana mahitaji yake.
MASWALI:
- Lengo la jaribu la kwanza lilikuwa lipi ?. Je, walishindaje jaribu?
- Taja maana ya vitu vilivyomo katika sanamu aliyoiona mfalme Nebukadneza.
- Matokeo ya ndoto aliyoota mfalme Nebukadneza ni:-
(a) _____________________________
(b) _____________________________
(c) _____________________________
(d) _____________________________
- Nini matokeo ya ushindi ya vijana watatu katika Danieli sura ya 3?
- Unapata fundisho gani kutokana na adhabu ambayo Mungu anayoitoa kwa mfalme Nebukadneza? (4:1-37)
- Ni dhambi gani aliyoifanya mfalme zbelshazar? (Dan. 1:1-3)
- Kuna faida zipi za mtu kumtegemea Mungu?
SOMO LA 3 : MTAWALA WA ULIMWENGU ANAYEKUJA:
A. MAONO YA WANYAMA WANNE (Dan. 7:1-28)
Lengo la 1: Linganisha ndoto ya Nebukadneza (2) na Maono ya Danieli – sura 7:
Kichwa cha Dhahabu Dan.2:37 | Simba mwenye mabawa matatu ya tai Dan.7:4 | Babeli Dan.2:37 |
Kifua na mikono ya fedha Dan. 2:39 | Dubu na mifupa mitatu ya mbavu kinywani – Dan. 7:5 | Uajemi Ilizishinda Misri, Ashuru, Babeli. Dan. 2:39 |
Tumbo na viuno vya shaba 2:39 | Chui mwenye mabawa manne 7:6 | Uyunani |
Miguu ya chuma 2:40 | Mnyama wa kutisha 7:7 | Rumi - 7:23 |
Nyayo nusu chuma, nusu udongo –2:41 | Pembe 10 na pembe ndogo 7:8 | Mataifa na Mpinga Kristo – 7:24 |
Jiwe lisilo kazi ya mwanadamu – 2:42 | Mfano wa Mwanadamu –7:13-14 | Yesu Kristo na Ufalme wa miaka elfu – 7:26-28 |
Maono haya yalionwa na Danieli wakati wa mfalme Belshazar. Maono haya yanayoonyesha kuwa mfumo wa utawala wa kibinadamu utatoweshwa na ufalme wa Mungu utasimamishwa milele. Kabla ya Yesu kutawala atakuja mpinga Kristo na kujitangaza kuwa mungu na kuwatesa watakatifu. Atatawala kwa miaka mitatu na nusu baada ya kuwaondoa wafalme 3 kati ya 10. Baada ya hapo ataangamizwa na Kristo kutawala pamoja na watakatifu .
B. MAONO YA KONDOO MUME NA BEBERU (MBUZI DUME) – Dan. 8:1-27.
Lengo la 2: Elezea vitu na mifano katika maono haya. Eleza umuhimu wake katika
unabii wa Kibiblia.
Maono ya yalionwa wakati wa mfalme Belshaza. Sura hii inaonyesha kuinuka na kuanguka kwa Dola za Uajemi na Uyunani.
1. KONDOO MUME – 539-333 KK – Ana pembe mbili ndefu ambazo ni Uajemi
na Umedi. Pembe ndefu zaidi ni Uajemi – utawala ulikuwa mkubwa.
2. BEBERU - 33 – 165 KK – Huyu ana pembe moja kati ya macho yake. Hii ni
Dola ya Uyunani ikiongozwa na Alexander- iliangusha ufalme wa Uajemi. Pembe nne zilizozuja ni wafalme waliozuka baa ya Alexander kufa.
(a) Kasanda - Makedonia
(b) Lysichus – Asia ya Kati
(c) Seleucus – Syria
(d) Ptolemy – Misri
3. Mfalme anayetokeza mwisho wa ufalme wa Uyunani ni Antonio Epifawe ambaye mkali, jeuri, mdanganyifu na mwenye nguvu. Alilinajisi hekalu la Mungu kwa kutoa vitu najisi. Lakini baada ya siku 2300 za dhabihu ya asubuhi na jioni (siku 1150) Antonio alitimuliwa katika mwaka 165 KK, hekalu likatakaswa.
C. MAOMBEZI YA DANIELI (Dan. 9:1-23)
Lengo la 3: Eleza umuhimu wa kuombea yale Mungu aliyoahidi kutimiza.
Katika mwaka wa kwanza wa kutawala mfalme Dario mwaka 539 KK. Danieli kwa kusoma vitabu aligundua kuwa myda wa utumwa wa miaka 70 umeisha kama alivyotabiri Nabii Yeremia, ili yatokee. Danieli anaomba na kutubu dhambi za watu wake. Matokeo ya maombi yake, Mungu anampa maono na maelezo ya majima Sabini.
Je, tunajifunza nini? Inatupasa kuombea mambo yale Mungu aliahidi kutufanyia ili yapate kutokea na kuonyesha zaidi yaliyoko mbele yetu.
D. MAJUMA SABINI -9:24-27
Lengo la 4: Fafanua haya Majuma Sabini:
1. Tangu kutolewa amri ya kujengwa mji na kuujenga itachukua majuma saba ambayo ni miaka 49 (Ezra na Nehemia)
2. Kipindi cha pili ni cha majuma 62 kutoka mji kujengwa hadi kukataliwa kwa Masihini miaka 434.
3. Kipindi cha mwisho ni juma moja lijalo wakati wa mpinga Kristo ambapo Mungu atashughulika na Israeli kama taifa. Israeli wataumiliki mji mtajkatifu katika kipindi cha kwanza cha miaka 3 na nusu na kipindi xha pili kitamilikiwa na watu wa mataifa (Ufu. 11:2). Israeli itateswa sana.
4. (a) Dan. 9:24-27 inahusika na watu wa Danieli na mji Mtakatifu maana yake
Israeli na mji wa Yerusalemu.
(b) Majuma Sabini ni miaka 490 iliyogawanywa sehemy kuu tatu:
Majuma 7 (miaka 49), majuma 62 (miaka 434), na juma moja (miaka 7)
(c) Kuangamizwa kwa mji na patakatifu pake ni mwaka 70 AD., ambapo
Warumi waliuangamiza Yerusalemu na hekalu lake.
(d) Danieli hakioni kipindi cha Kanisa kwa sababu Mungu alitaka aonyeshwe
mambo yanayohusiana na taifa la Israeli.
5. Katika Juma la 70 Wana-Israeli
(a) Watafanya agano na mpinga Kristo
(b) Baada ya miaka 3 na nusu agano litavunjika, mpinga Kristo ataondoa
uhuru wa kuabudu.
(c) Kutokana na mateso mwatamhitaji Masihi.
6. Katika Majuma 70 mambo haya yatafanyika kwa ajili ya Yerusalemu na Israeli
(a) Kukomesha dhambi
(b) Kusamehe uovu
(c) Kuleta haki ya milele
(d) Kutia mhuri maono na unabii
(e) Kupaka mafuta patakatifu sana.
- MARUDIO NA MAPIITIO:
Lengo la 5: Eleza jinsi maendeleo ya Ufunuo katika Dan. 2,7,8,9,na umuhimu Wake.
Maendeleo ya ufunuo katika Dan. Sura 2,7,8,9, inaanzia kwenye maelezo ya jumla katika sura ya 2 na katika sura zingine tunaelezwa kwa undani zaidi jinsi mambo yatakavyokuwa. Umuhimu wa maendeleo ya ufunuo hatua kwa hatua unatufundisha kuwa ili tuipate kweli lazima tusome na kupiitia sura yote.
MASWALI:
- Chora jedwali na ulinganishe ndoto ya mfalme Nebukadneza (Dan. 2:1-42) na maono ya Danieli katika sura ya saba.
- Katika Dan. 8:1-27
(a) Kondoo mume ni nani?
(b) Beberu ni nani?
- Je, kuna umuhimu gani wa kuombea mambo ambayo Mungu ameahidi kutufanyia?
- Chora mchoro unaofafanua majuma Sabini.
SOMO LA 4: SIKU ZIJAZO ZA TAABU:
A. UTUKUFU WA YESU KRISTO.
Lengo la 1: Taja vitu vinavyofanana na maono aliyoyaona Yohana katika Ufunuo na yale ya Dan.10:5,6.
VITU | DANIELI | UFUNUO | MAANA |
Mavazi | Nguo za Kitani (Mst.5) | Vazi lililofika miguuni (Mst.13) | Hekima |
Mshipi | Dhahabu (Mst.5) | Dhahabu (Mst. 13 | Thamani mno. |
Macho | Taa za moto (Mst.6) | Mwali wa moto (Mst.14) | Ana uwezo wa kuona |
Sehemu ya chini | Rangi kama ya shaba (Mst.6) | Shaba iliyosuguliwa (Mst.15) | Imara |
Sauti | Kama ya umati wa watu (Mst.6) | Ya maji mengi (Mst.15) | Mamlaka na Nguvu |
Umuhimu wa maono haya yalikuwa na lengo lifuatalo:
1. Kuwatia moyo na kuwapasha watu wa Mungu juu ya mambo yajayo
2. Maono haya yalimpa kuelewa yale yaliyotabiriwa muda yatakapotimia.
3. Maono haya yalikuwa jibu la maombi ya Danieli ya muda wa siku 21.
Maono haya Danieli aliyapata mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Koreshi wa Uajemi.
B. MAPAMBANO YA KIROHO –Da. 10:13-21.
Lengo la 2: Elezea vita vya Kiroho vinavyofunuliwa katika sura hii.
Sura hii inatoa mfano wa upinzani dhidi ya Mungu unaotawala katika anga hili. Majibu ya maombi ya watumishi yanacheleweshwa kutokana na upinzani wa wakuu wa giza wanaowapinga malaika watakatifu waletao majibu. Asifiwe Bwana kwani hakuna mamlaka inayoweza kuzuia maombi yetu kwenda kwa Mungu. Tukivumilia majibu yanaweza kuletwa. Katika sura hizi tunajifunza kuwa kuna malaika wa Mungu wanaosimama kwa niaba ya mataifa wakiongozwa na Mikaeli.
C. MTIRIRIKO WA HISTORIA KUTOKA DOLA YA UAJEMI NA UMEDI HADI MWISHO WA NYAKATI.
1. UAJEMI NA UYUNANI (Dan.11:1-4)
Lengo la 3: Onyesha mambo muhimu katika unabii kuhusiana na Uajemi na Uyunani.
Wafalme wane:
(a) Koreshi – 539 –529 KK – miaka10 (Ezra 1:1)
(b) Artashasta – 529 – 522 KK – miaka 7 (Ezra 4:7.)
(c) Ahasuero (Xerxes)
(Dario Hystaspes) – 521 – 486 KK – miaka 35 (Esta 1:1)
(d) Eexes I – 486 – 468 KK – miaka 18.
(Huyu ndiye aliyekuwa tajiri kuliko wafalme wote. Utajiri wake na jeshi la watu 800,000 lilimchochea kupigana na Wayunani. Katika vita hivi alishindwa vibaya na Wayunani au Wagriki. Dola ya Uajemi ilidumu kwa miaka 200 (Mst.3,4) – 538 – 333 KK.Mfalme hodari ni Alexander wa Ugriki aliyeupindua na kuangusha dola ya Uajemi katika mwaka 333. Alifariki mwaka 323 KK bila kuwa na wana wa kutawala. Dola ya Ugriki iligawanyika katika sehemu kuu nne chini ya wakuu wa majeshi:
(i) Kasanda - Makedonia
(ii) Lysmauhus – Asia
(iii) Selukia – Syria
(iv) Ptolemy – Misri
N.B: Katika unabii wa sura wafalme wawili wanahusika:
-Selukia wa Syria (Mfalme wa Kaskazini)
-Ptolemy wa Misri (mfalme wa Kusini)
2. FALME ZA PTOLEMY NA SELUKIA HADI ANTIOKIA EPIFANE –Dan.11:5-20.
Lengo la 4: Eleza umuhimu wa Ptolemy na Selukia katika historia ya Biblia.
Hawa ni muhimu kwa sananu Israeli ilikuwa kati ya Falme hizi mbili, hivyo ilihusika sana katika historia yao. Kati ya 323 –178 KK Israeli ilitawaliwa na Ptolemy mfalme wa Kusini. Hivyo tuangalie unabii ulivyotumia.
Mst. 5: Ptolemy I lagus au Soster ni mfalme wa Kusini aliyetawala Misri, Arabia, Libya, Ethiopia n.k. Selukia I (mshindi) Nikano alikuwa mfalme wa Kaskazini.
Mst. 6: Ptolemy II Philadephus alimwoza binti yake Berenise kwa Selukia Antiokia II Theoss mwenye mke aitwaye Laodice, ili kuleta mapatano. Baada ya kifo cha mfalme wa Kusini, Antiokia alimtaliki Berenice na kumrudia mkewe Laodice. Baadaye Laodice akamuua mume wake kwa sumu na kuwuua Berenice na mtoto wake. Hivyo mtoto wa Laodice Seleukia Callinicus akatawala.
Mst. 7-9 Ptolemy III Euergette akamshambulia Seleukia Callinicus na kumshinda na kuteka mateka ili kulipiza kisasi.
Mst.10-12 Wana wa mfalme wa Kaskazini ni Selecus (mkubwa aliyeuwawa kwa sumu na Antiokia aliyetawala kwa miaka 37. Akashambulia Misri akashindwa na Ptolemy Epifanes.
Mst.13-16 Akishirikiana na waasi wa Kiyahudi, Antiokia akamshinda mfalme wa Kusini na kuimiliki Israeli.
Mst. 17 Antiokia III baada ya ushindi alimpa Ptolemy Epifane dada yake Cleoptra awe mkewe.
Mst.18-19 Antiokia III alitanua ufalme wake hadi Asia ya Kati na kushindwa na Warumi wakiongozwa na Seipto.
Mst. 20: Seleukia Philopater alitawala na kutoza Kodi kwa ukatili akauwawa kwa sumu na mtumishi wake Heliodorus.
Je, tunajifunza nini? Mungu ndiye anaweka na kung’oa wafalme atakavyoYeye.
3. ANTIOKIA EPIFANE –Dan.11:21-45
Lengo la 5: Eleza mambo muhimu ya unabii kuhusiana na Antiokia Epifane
aliyotumia katika Historia.
Mst. 21 – Tabia yake Antiokia Epifane alikuwa mdanganyifu, mwenye kiburi na mjanja. Yeye alikuwa amewekwa ndani huko Rumi. Alipata ufalme kwa hila alimfanya mtoto wa kaka yake Demeterio kuwa mfungwa badala yake. Akatawala Syria kwa kujidai anamshikia madaraka kwa kitambo kidogo.
Mst. 22-24 – Hata shika mapatano yake bali akishirikiana na watu wachache atavamia Mikoa tayari na kuteka mali ambayo aliwahawia rafiki zake.
Mst. 25-28 – Antiokia Epifane atakusanya majeshi na kumshambulia mfalme wa Kusini na kumshinda Ptolemy Philometer na kufanya mkataba ambao haukudumu.
Mst. 29-30 – Alivamia tena ufalme wa Kusini, lakini wakati huu alishindwa kwa Ptolemy Philometer akisaidiwa na Warumi. Warumi walimwamuru Antiokia kuondoa majeshi yake.
Mst. 31-35 – Baada ya kurudi kutoma Misri huku ameshinea, hasira zake alizielekeza kwa Wayahudi na kuondoa shughuli za Ibada katika Hekalu. Alifanya hivi akisaidiwa na Wayahudi waasi. Akalinajisi hekalu kwa kutoa vitu vilivyonajisi. Wayahudi wengine waliowaaminifu walishikilia Imani yao, Wengi kati yao waliuawa.
Mst. 36-39 – Antiokia Epifane alimkufuru Mungu Aliye juu kwa kuondoa dhabihu zake na kunajisi Sabato, hekalu na watu wa Mungu. Pia alidharau miungu na baba zake na kuleta miungu ya kigeni ya Wayunani (Jupiter olympius)
Mst. 40-43 – Mfalme wa mwisho Kusini alivamia tena utawala wa Antiokia Epifane , lakini alishindwa tena. Mfalme wa Kaskazini aliteka mali nyingi ya Wamisri.
Mst. 44-45 – Habari za maadui kutoka Mashariki na Kaskazini ni majeshi Waajemi na Waapathi zikamsumbua. Akaingia na kuwateka Wayahudi. Lakini aliugua ugonjwa usioponyeka na kufa.
N.B: Antiokia Wpifane alikuwa kivuli cha mpinga Kristo atakayekuja.
FALME MBILI:
KUSINI (Ptolemy) KASKAZINI (Seleukia)
Ptolemy I Soster –323 –285 Seleukia Nicator – 312-280
Ptolemy II Philadelphus –285-246 Antiokia I Sater – 280-261
Ptolemy III Euergetes – 246 – 221 Antiokia II (Theos) – 261 –246
Ptolemy IV Philopator – 221 –204 Selukia II Callinicus –246-226
Ptolemy V – Epifane – 204 – 181 Selukia III Ceranus –226-223
Ptolemy VI Philometa –181-145 Antiokia III 223-187
Selukia IV –187-175
Antiokia IV Epifane –175-164
D. WAKATI WA TAABU – Dan. 11:36-12:13
Lengo la 6: Taja ushahidi ambao unayaweka matukio yaliyomo katika Danieli 12 kutoka katika Juma la Sabini.
Dan 11:36 – 45 inazungumzia juu ya kutokea kwa mpinga Kristo atakaye vamia taifa la Israel na kujitangaza kwamba yeye ni Mungu anayetakiwa kuabudiwa.Atafanya kazi kwa miaka mitatu na nusu baadaye kuangamizwa.
Ushahidi katika sura 12 unaonyesha kuwa wakati wa taabu utatokea katika kipindi nusu ya pili ya juma la Sabini. Kipindi hicho kitakuwa cha miaka 3 na nusu. Kipindi hicho kitaanza wakati mpinga Kristo amevunja mkataba wa amani na Wayahudi.
Matukio ya wiki ya sabini ni kama ifuatavyo:-
1. Kitaanzishwa na ujio wa mpinga Kristo atakayeongoza mataifa kumi.
2. Ataweka mkataba wa amani na Wayahudi wa miaka saba. Baada ya miaka 3 na nusu mkataba utavunjwa.
3. Atawageukia Wayahudi na kuwatesa kwa lengo la kuwaangamiza, lakini malaika Mikaeli atawasaidia na watakatifu kuokolewa.
4. Kabla ya Mungu kuanzisha ufalme wake ataondosha utawala wa mpinga Kristo.
5. Watakatifu waovu watafufuliwa kuingia katika aibu na watakatifu katika baraka ya milele.
MUHTASARI WA MATUKIO MUHIMU:
605 KK – Mateka wa kwanza kupelekwa Babeli akiwemo Danieli na rafiki zake
597 KK – Mateka wengine wapelekwa Babeli akiwemo Ezekieli
587 KK – Yerusalemu uliangamizwa na watu kupelekwa utumwani Babeli.
587 KK – Koreshi anakuwa mfalme wa Uajemi.
550 KK – Uajemi yaishinda Umedi
539 K K – Uajemi yaishinda Babeli
538 KK – Kundi la kwanza la Wayahudi wakiongozwa na Zerubabeli warudi Yerusalemu. Kazi ya ujuzi wa Hekalu yaanza
516 KK – Hekalu laisha kujengwa.
458 KK – Wakiongozwa na Ezra Wayahudi kundi la pili warudi Yerusalemu.
445 KK – Nehemia aenda Yerusalemu kama Gavana
333 KK – Alexander Mkuu aishinda Uajemi
323 KK – Dola ya Ugriki inagawanyika katika sehemu nne.
301-198 – Palestina ilitawaliwa na Misri (Ptolemy)
198 –143 – Palestina ilitawaliwa na Syria (Seleukia)
171 KK – Antiokia Epifane anakuwa mfalme wa Syria
168 KK – Antiokia Epifane alinajisi Hekalu la Wayahudi
165 KK – Wayahudi waliongozwa na Makabayo wanalikomboa Hekalu.
145 KK – Palestina yapata uhuru.
63 - Dola ya Rumi wateka Palestina
6 - Kuzaliwa kwa Yesu
31 BK – Kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo
70 BK - Kuangamizwa kwa Yerusalemu na Warumi.
MASWALI:
- Umuhimu wa maono ya sura ya 10 ulikuwa una lengo lifuatalo:
(a) ______________________
(b) ______________________
(c) ______________________
- Katika sura ya 10:13-21 kuna vitu gani vya kiroho vinavyofunuliwa?
- Taja mambo ambayo wafalme hawa waliwafanyia Wayahudi:
(a) Koreshi ____________________________
(b) Artashasta _________________________
(c) Ahasuero __________________________
- Antiokia Epifane anakumbukwa kwa matendo gani aliyowatendea Wayahudi?
- Taja matukio matano yatakayotokea katika juma la Sabini.
_______________________________________________________________________________________________________________
About JAMPHINA BLOG
0 $type={blogger}:
Post a Comment